20 Dec 2015
HIZI NDIZO SABABU ZILIZO MPONZA DK. MWAKA MPAKA KUPELEKEA KUTEMBELEWA NA NAIBU WAZIRI DK. KIGWANGALLA.
Sakata la mmiliki wa Kliniki ya Tiba Asilia ya Fore Plan iliyopo Ilala Bungoni, Dar, Dk. Juma Mwaka ‘JJ Mwaka’ kufanyiwa ziara ya kushtukiza na baadaye kudaiwa kumkimbia Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Hamis Kigwangalla limechukua sura mpya huku mambo mengi yaliyomponza yakifichuka.
MAMBO YALIVYOKUA
Siku chache baada ya kuteuliwa kuwa naibu waziri, Dk. Kigwangalla alifanya ziara ya kushtukiza katika kituo hicho kinachosifika kwa kutoa tiba ya asili badala ya hospitali (tiba mbadala), hasa kwa wanawake wanaosumbuliwa na matatizo ya uzazi.
Katika hali ya kushangaza, matatibu na manesi waliokuwa kazini walitokomea kusikojulikana na kuwatelekeza wagonjwa, wakikwepa kuonana na waziri huyo ambaye akiwa na msafara wake, walifanya ukaguzi wa kina kwenye kituo hicho.
Kufuatia kitendo cha Dk. Mwaka na wenzake kuingia mitini, Waziri Kigwangalla alitoa amri ya kufungwa kwa muda kwa kituo hicho mpaka uchunguzi wa kina utakapokamilika ili kuona kama huduma zinazotolewa zinakidhi vigezo na ni salama kwa wagonjwa.
Naibu waziri, Dk. Kigwangalla akikagua baadhi ya dawa kwenye hospital ya Dr. Mwaka.
MITANDAO
Simulizi ya jinsi tabibu huyo alivyosimamishwa kutoa huduma ili kupisha uchunguzi na ukaguzi wa kina, inaanzia mbali ambapo kwa mujibu wa vyanzo vyetu vya kuaminika, chokochoko kuhusu huduma zake zilianzia kwenye mitandao ya kijamii.
“Kwa kipindi kirefu kulikuwa na makundi mawili yanayoshindana kwenye mitandao ya kijamii. Kundi la kwanza ni wale waliowahi kutibiwa katika kliniki hiyo na kufanikiwa kupona matatizo yao.
“Hawa walikuwa wakimtetea kwamba anatoa huduma sahihi lakini kundi jingine ni wale waliotibiwa na kupoteza fedha nyingi bila kupona matatizo yaliyokuwa yakiwasumbua.
“Hawa ndiyo waliochangia kwa kiasi kikubwa kuifumbua macho Serikali ya Rais John Pombe Magufuli kwani walitaka dawa na huduma za Dk. Mwaka zichunguzwe kwa vile walishapoteza imani naye,” kilisema chanzo chetu makini kwa sharti la kutoandikwa jina gazetini.
KUANIKA MAISHA YAKE MTANDAONI
Kwa mujibu wa chanzo kingine, tabia ya Dk. Mwaka kupenda kuanika maisha yake kwenye mitandao ya kijamii ni suala jingine lililomponza na kufanya watu waanze kutilia shaka utajiri wake.
“Unajua Dk. Mwaka na mkewe wamekuwa wakiposti kwenye mitandao ya kijamii, hasa Instagram picha za magari yao ya kifahari anayomiliki likiwemo Range Rover-Sport SE na hekalu (jumba kubwa la ghorofa) analoishi, lipo Mbezi (Dar).
“Pia walikuwa na kawaida ya kujisifia wanaposafiri kwenda nje ya nchi kufanya shopping, hasa Dubai. Hicho pia kimemponza sana maana watu walianza kufuatilia utajiri wao na pengine ndiyo waliomchongea serikalini,” kilisema chanzo hicho kilicho karibu na familia hiyo.
Baadhi ya mali anazo miliki Dk Mwaka.
VIPINDI KWENYE RUNINGA
Sababu nyingine inayotajwa na vyanzo vyetu kwamba imemponza tabibu huyo, ni ile kawaida yake ya kuendesha vipindi kwenye runinga, akieleza huduma anazozitoa kwa lengo la kupata wateja wengi.
“Unajua Dokta Mwaka ndiye anayeongoza kwa kuwa na vipindi vingi vya runinga kwenye televisheni mbalimbali nchini. Kama unavyojua kipindi kimoja cha runinga kulipia kinagharimu fedha nyingi sana. Sasa watu wakawa wanajiuliza anapata wapi fedha za kulipia gharama hizo? Ni kutoka kwa wateja wake kweli?” kilisema chanzo chetu.
Dk Mwaka akiwa katika moja ya vipindi vyake kwenye runinga.
KUPUUZA AGIZO LA WIZARA
Pia, habari za ndani zinadai kuwa, mwaka jana wizara husika iliwaita wataalam wote wanaotoa tiba mbadala na kuwapa masharti.
Masharti hayo ni kutovaa koti jeupe, kutoning’iniza shingoni chombo cha kusikilizia mapafu/mapigo ya moyo (stethoscope) na kutojiita madaktari wakitakiwa kutumia utambulisho wa tabibu masharti ambayo karibu wote wameyapuuza.
JE, KUNAKOSA KUJITANGAZA?
Katika utafiti uliofanywa na gazeti hili na kutiliwa nguvu na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu imebainika kwamba, kwa mujibu wa viapo wanavyokula madaktari na matabibu ni makosa kujitangaza kwenye redio, runinga au mitandao kwa lengo la kuwavuta wagonjwa.
“Changamoto iliyopo kwetu ni kwamba matangazo wanayoyatoa ni kinyume na kanuni lakini tumebaini kwamba Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ambayo inasimamia sekta ya mawasiliano na utangazaji nchini ndiyo inayoruhusu. Tumejipanga kukutana nao ili kujadili jambo hili,” alisema Mwalimu.
SIO MARA YA KWANZA KUFUNGIWA
Tukio hili la kusimamishwa kutoa huduma, si la kwanza kumtokea Dk. Mwaka ambapo mwaka jana, maafisa kutoka wizara ya afya walifika kwenye kliniki hiyo kwa kushtukiza, wakiwa wameongozana na waandishi wa habari na kufanya ukaguzi ambapo kutokana na kutoridhishwa na mazingira waliyoyakuta, walilazimika kuifunga kliniki hiyo kwa muda usiojulikana.
Hata hivyo, wiki kadhaa baadaye, Dk. Mwaka alifungua kesi mahakamani kupinga kufungiwa huko na kushinda kesi.
Dk Mwaka akiwa na msanii Diamond Platinum.
Source: Globalpublishers.com (story by Deogratius Mongela na Chande Abdallah).
0 comments:
Post a Comment