11 Aug 2016

HIZI NDIZO MBINU 6 KUBWA ZITAKAZO KUSAIDIA KUPATA AJIRA MAPEMA NA KWA URAHISI.

Ni ukweli usiofichika kwamba hakuna jambo muhimu maishani kama kuwa na kazi inayokuingizia kipato.
Hata hivyo, ni lazima pia tukubaliane kwamba si kazi nyepesi kupata kazi. Sote ni mashahidi wa jinsi watu wanavyohangaika mitaani kutafuta kazi, hata kama wamesoma na wana ujuzi wa kutosha.
Sote ni mashahidi pia wa jinsi baadhi ya watu wanavyochanganyikiwa wanapoishi muda mrefu bila kuwa na kazi.
Wengi hupatwa na vichaa na wengine kujiingiza katika ulevi wa kupindukia na utumiaji dawa za kulevya kutokana na kukata tamaa ya maisha kwa kukosa kazi.
Hii inatokana na watu wengi kukosa elimu ya namna  wanavyoweza kutumia vizuri muda wao wa dhahabu wanapokuwa hawana kazi kwa sababu mkosa ajira huathirika endapo atashindwa kutumia muda wa awali kujiokoa na makucha ya kukosa kazi.
Ni rahisi kupata kazi muda mfupi baada ya kumaliza shule  au kufukuzwa kazi kuliko kukaa nje ya ajira (kijiweni) kwa miaka sita au saba.
Kimsingi kuna maangalizo mengi katika mada hii ambayo watu wasiokuwa na ajira wanatakiwa kuzingatia lakini kwa uchache tutaangalia yale ambayo ni muhimu kufuatwa na watafuta ajira ili waweze kufanikiwa kirahisi na kuepuka madhara ya kisaikolojia na kutopata kazi.

KUTULIZA AKILI
Inashauriwa kuwa muda mfupi baada ya kufutwa kazi au kumaliza masomo na kukutana na vikwazo vya awali vya kukosa kazi, mhusika hatakiwi kuwa na taharuki kwa kuanza kunywa pombe, kustarehe, kuwa na msongo wa mawazo, bali unatakiwa kutulia na kuendelea kushikamana na wafanyakazi wenzake wa awali, wanafunzi waliomaliza naye shule na watu ambao wako kwenye mtandao wa kazi ili kujiweka katika mazingira ya kuokoka ndani ya muda muafaka.

KUJITAMBUA
Mkosa ajira anatakiwa kujitambua kuwa yeye ni nani na kuhakikisha kuwa maisha yake yanakwenda kama yeye alivyo. Mhusika anatakiwa kutunza kumbukumbu zote za elimu yake kama vyeti na kuwa hai kila siku katika ujuzi wake. Pia haifai kuwa na aibu kwa kujiona duni, ni vema kuwa na imani kuwa kipindi cha kukosa ajira ni cha muda mfupi.

KUJITAMBULISHA
Muda wa awali ambao mtu atakuwa hana kazi ni muhimu sana kwake kufanya utambulisho kwa rafiki zake, ahakikishe kuwa watu wanaweza kuwasiliana naye kwa urahisi. Si busara kujifungia chumbani na kuzima simu, kufanya hivyo kunaweza kuwafanya rafiki zako washindwe kukupa dokezo za nafasi za kazi na hata kukusahau kabisa.

KUWA TAYARI
Unapokuwa huna ajira ni lazima uwe tayari wakati wote kwa kuanza kazi, isiwe unaambiwa kazi imepatikana unaanza kusema “sina vyeti, viko kwa bibi” muda wa dhahabu lazima utumike vizuri ili kutopoteza muda wa kujikomboa. Ni muhimu pia kuandaa CV yako na kuwa nayo kwenye kabati ili itakapohitajika usipoteze muda kuiandaa!

USIULEMAZE MWILI
Kuna watu ambao huchelewa kuamka au kushinda wamelala kwa sababu hawana kazi za kufanya, jambo ambalo ni hatari kwa afya. Hata kama ukosefu wa ajira unakuumiza kiasi gani usikubali kubweteka kwa kulala, utumikishe mwili pengine hata kwa kazi ambazo si za masilahi makubwa. Haifai kulazimisha sana ajira kwa kuwaganda mabosi.

USIKATE TAMAA
Kifupi hatua hizi ni muongozo wa kuweza kutumia muda wa dhahabu katika kupata kazi, hata hivyo mtu hatakiwi kukata tamaa ya kutafuta kazi ingawa ukweli utabaki kuwa kadiri unavyozidi kuchelewa kupata kazi kwa miaka mingi ndivyo anavyozidi kuweka mazingira magumu ya kuajiriwa. Hivyo ni bora ukahangaika mapema kwa kutumia uwezo na mbinu zote ili kuepuka kupotea katika ulimwengu wa ajira na kujikuta umeathirika kisaikolojia.
Nimatumaini yangu, wewe msomaji na mtafutaji ajira utaweza kuzifuata mbinu hizi na kufanikiwa.
Kilaraheli!


0 comments:

Post a Comment